Wanariadha Chipukizi Huenda Wakatumia Dawa Za Kusisimua Misuli

Wanariadha chipukizi wa humu nchini huenda wakatumia dawa za kusisimua misuli kwa sababu hawafahamu wala kuelewa vyema sheria za utumizi wa dawa haramu michezoni. Haya ni kulingana na mwenyekiti wa chama cha riadha Kenya Jackson Tuwei, aliyekuwa akiwahutubia wanariadha mashuhuri wa humu nchini huko Eldoret, walipokuwa wakifanyiwa uchunguzi wa dawa haramu na chama cha madaktari kilichozinduliwa. A�Baadhi ya wanariadha wa Kenya wamejipata matatani na shirikisho la kupambana na utumizi wa dawa haramu michezoni WADA, kwa sababu ya kuwapo kwa idadi kubwa ya wanariadha waliopatikana wakitumia dawa hizo. Hata hivyo katika juhudi za kuhakikisha kuwa wanariadha wa humu nchini hawatumii dawa hizo, chama cha riadha Kenya kilizindua semina mjini Eldoret, iliyowavutia wanariadha 108 wa humu nchini. Lengo kuu la semina hiyo ni kuanzisha mradi ambapo madaktari 6 watawachunguza wanariadha wa humu nchini kabla hawajashiriki katika mashindano ya kimataifa. Mwaka jana, shirikisho la riadha duniani, IAAF, lilitoa tahadhari kwa wanariadha wa Kenya kwa sababu ya idadi inayoongezeka ya utumizi wa dawa haramu, huku zaidi ya wanariadha 40 wakiwa tayari wamepigwa marufuku ya muda kuanzia mwaka 2012. A�