Matiang’i awaongoza maafisa wa wizara ya elimu kwa uangalizi wa mtihani

Waziri wa elimu, Dr. Fred Matianga��i, leo aliwaongoza maafisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo kwenye shughuli ya uangalizi wa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane ulioanza leo na ambao utakamilika siku ya Alhamisi. Dr Matiangi aliwasili mjini Wote katika kaunti ya Makueni ambapo alishuhudia kufunguliwa kwa makasha yaliyohifadhi karatasi za mtihani huo mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri kabla ya kutembelea shule kadhaa katika kaunti hiyo. Mwenzake wa teknolojia ya mawasiliano Joe Mucheru alizuru kaunti ya Nyeri ilhali waziri wa jinsia na masuala ya vijana, Sicily Kariuki aliongoza shughuli hiyo katika kaunti ya Kiambu. Afisa mkuu mtendaji wa tume ya kuwaajiri walimu, Nancy Macharia naye aliongoza shughuli hiyo katika eneo la Isinya, kaunti ya Kajiado huku mwenyekiti wa baraza la kitaifa la mitihani, Profesa George Magoha na afisa mkuu mtendaji wa taasisi ya ustawishaji mtala wa elimu Dr. Julius Jwan wakizuru kaunti za Migori na Homa Bay mtawalia.