Matiangi Awahimiza Wazazi Kuzingatia Kozi Za Kiufundi Kwa Watoto Wao

Waziri wa elimu Dkt. Fred Matianga��i amewahimiza wazazi kuzingatia kozi ya kiufundi na sayansi kwa watoto wao badala ya zile za usanii na masuala ya kijamii. Waziri wa elimu alisema nchi hii haiwezi kupata ufanisi ikiwa asilimia 80 ya wanafunzi watajisajili katika vyuo vikuu na vyuo vingine kufanya kozi na masomo ya sanaa. Akiongea leo wakati wa uzinduzi wa mpango wa banki ya Equity wa Wings to Fly, katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Matiangi alisema dhana kwamba kozi za mafunzo ya anwai sio za kifahari ni la kupotosha. Kadhalika alifichua kwamba bodi ya kutoa mikopo ya elimu ya juu HELB itakuwa ikitoa fedha zaidi kwa wanafunzi wanaosomea kozi za kisayansi tofauti na wenzao wanaosomea kozi za masomo ya sanaa. Hafla hiyo ilishuhudia karibu wanafunzi elfu 3 waliofuzu kufadhiliwa na mpango wa Wings to Fly ambao walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wakijiunga na vyuo vya mafunzo ya anwai kote nchini. Nchi hii ina zaidi ya vyuo 60 vya kibinafsi na umma vya mafunzo ya anwai na vingine 70 vinajengwa ambavyo vinatoa kozi mbali ikiwa ni pamoja na zile za viwango vya vyeti na stashahada.