Mashauriano zaidi yahitajika kabla kuanzisha mtalaa mpya wa elimu

Katibu mkuu wa chama cha kitaifa cha walimu, KNUT, Wilson Sossion amesema kuwa mashauriano zaidi yanahitajika kabla ya kuanzisha mtalaa mpya wa elimu mwaka ujao. Akiongea jana wakati wa mkutano wa kila mwaka wa walimu wakuu uliofanyika jijini Mombasa, Sossion alisema kuwa muda zaidi unahitajika kufanyia majaribio na kuidhinisha mtalaa huo mpya. Alisema kuwa marekebisho ya mtalaa ni sharti yapitie hatua zinazofaa ambazo ni tathmini, kuratibu sera, kubuni mfumo wa mtalaa huo, kubuni silabasi, vifaa vya ufundishaji na pia vifaa hivyo vinafaa kufanyiwa majaribio na kuthibitishwa kwamba vinaweza kutumika kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo. Hata hivyo Sossion alisema kuwa hapingi mtalaa huo mpya lakini ni muhimu kwa miradi ya kutosha ya kimajaribio kutekelezwa ili kutathmini ubora wake kabla ya kuuanzisha. Waziri wa elimu Fred Matiangi tayari amesema kuwa mtalaa huo mpya utaanzishwa mwaka ujao. Mfumo huo umegawanywa katika makundi matatu ambayo ni elimu ya chekechea kuanzia nasari hadi gredi ya tatu, kiwango cha kadri kuanzia gredi ya nne hadi ya tisa na kiwango cha juu kuanzia gredi ya 10 hadi ya 12.