Maseneta wataka wizara ya fedha kutii muda uliowekwa wa kusambaza fedha

Maseneta wametaka wizara ya fedha kutii muda uliowekwa kila mara inaposambaza fedha kwa serikali za Kaunti.  Hali hiyo, wamesema itaweza kuepusha visa ambapo miradi haikamilishwi katika muda uliowekwa kutokana na ukosefu wa fedha.  Wakitoa maoni  kuhusu ripoti ya msimamizi wa bajeti  kuhusu bajeti za serikali za kaunti  za mwaka wa matumizi  ya fedha 2016-2017, maseneta  Amos Wako [Busia], Hargura Godana [Marsabit],  na  Fatuma Dullo [Isiolo]  walisema  kuna haja ya  kuongeza kiwango cha uwajibikaji  katika usimamizi wa rasilimali za umma ili kuwezesha matumizi bora ya fedha. Wako alishangazwa na habari kwamba baadhi ya serikali za kaunti zimeshindwa kukusanya ushuru kikamilifu jinsi ilivyokadiriwa kwenye bajeti zake.  Alisema hali hiyo imechangia utoaji duni wa huduma licha ya kuwepo mfumo wa ugatuzi. Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo kwa upande wake alisema kuna haja ya kuhakiksha kauli zote za bunge la seneti zinatekelezwa.