Marufuku ya NTSA yatatiza safari kutoka mashambani

Wanafunzi wengi hawangefika shuleni jana kama ilivyopangwa hasa wale waliodhamiria kusafiri usiku kwa mabasi kutoka sehemu mbali mbali za nchi. Hii inafuatia uamuzi wa halmashauri ya taifa ya uchukuzi na usalama barabarani siku ya Jumapili wa kupiga marufuku kwa muda usiojulikana safari za usiku za magari ya uchukuzi wa abiria kufuatia kuongezeka kwa maafa ya ajali za barabarani.

Jana usiku wasafiri wengi, baadhi yao wakiwa wanafunzi ambao walikuwa wakirejea shuleni kote nchini, walikwama katika vituo mbali mbali vya mabasi huku marufuku hiyo ya safari za usiku za magari ya uchukuzi wa umma ikiendelea kutekelezwa. Shule kote nchini zilitarajiwa kufunguliwa jana na leo. Wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma sasa wanalalamika kwamba wamelazimika kukabiliana na changamoto mbali mbali kutokana na marufuku hiyo ya safari za usiku wakisema wanapata hasara kwani wasafiri wanawalazimu kuwapa usafiri mbadala.