Marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki kuanza kutekelezwa tarehe 28 Agosti

Katibu katika wizara ya mazingira, Charles Sunkuli amesema makataa ya marufuku dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki yanayomalizika Jumatatu tarehe 28 mwezi huu hayatabadilishwa licha ya malalamishi ya watengenezaji bidhaa hiyo. Katibu huyo alisema marufuku hiyo inaambatana na katiba ambayo inampa kila mkenya haki ya kuishi katika mazingira safi. Akiongea jana na wanahabari, Sunkuli alisema tayari serikali imechukua hatua za kupunguza utengenezaji au uagizaji wa mifuko ya plastiki na inashirikiana na serikali za kaunti kubuni sera kuhusu kupunguzwa kwa matumizi ya mifuko hiyo. Sunkuli alihimiza serikali za kaunti kuhakikisha zimebuni sheria za kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki. Alisema wakenya hawana budi ila kutafuta njia mbadala za kubeba bidhaa kwa lengo la kuhifadhi mazingira.A�Watengenezaji bidhaa wamedai kwamba marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki itaathiri moja kwa moja takriban nyadhifa elfu-60 na nyingine laki 4 zisizokuwa za moja kwa moja, madai ambayo serikali imeyakanusha ikisema mikakati kabambe imewekwa ili kuwalinda.