Marubani Wa KQ Wataka MKurugenzi Mkuu Aondoke

Maafisa wa serikali wanashauriana na wasimamizi wa shirika la Kenya na waakilishi wa chama cha marubani kutatua mzozo kati ya shirika hilo na marubani wake. Mkutano huo umejiri huku marubani wakisisitiza kuwa watagoma kuanzia kesho wakilalamika kuwa wasimamizi wa shirika hilo wameshindwa kudhibiti hali ya kifedha ya shirika hilo. Serikali tayari imeashiria kuwa afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo, Mbuvi Ngunze na mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo, Denis Awori wataondoka afisini hivi karibuni. Hata hivyo marubani hao wanataka wawili hao waandike barua za kuthibitisha kujiuzulu kwao. Waziri wa uchukuzi James Macharia anaongoza mkutano huo unaotafuta suluhu kwa mzozo huo. Hapo jana, safari za ndege za shirika hilo zilichelewa kwa muda mrefu baada ya wahudumu wa ndege wa muda kugoma. Bunge la taifa pia limekuwa likihimiza mabadiliko kwenye shirika hilo.