Marekani yapongeza kuchaguliwa kwa Rais Kenyatta

Marekani imeungana na mataifa mengine duniani kumpongeza rais Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa Kenya lakini ikasema imefadhaishwa na purukushani zilizokumba baadhi ya maeneo hapa nchini. Kwenye taarifa, ubalozi wa Marekani jijini Nairobi umesema umefurahia wito wa rais Kenyatta wa kudumishwa kwa amani na umoja hapa nchini. Ujumbe mwingine wa pongezi umetoka kwa rais Xi Jinping wa China ambaye alisema nchi yake itashirikiana na Kenya katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya raia wao. Naye waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alimpongeza rais Kenyatta kwa ushindi wake na kuahidi kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika nyanja za kilimo na usalama. Muungano wa Ulaya kupitia naibu wake wa rais anayehusika na maswala ya kigeni, Federica Mogherini ulitaja uchaguzi huo kuwa huru na wa haki. Muungano huo wa Ulaya umejitolea kushirikiana na Kenya katika ajenda yake ya maendeleo kwa ajili ya kwa ufanisi wa nchi hii.