Marekani Yatetea Hatua Yake Kupinga Makazi Mapya Ya Wayahudi Ukingo Wa Magharibi Mwa Mto Jordan

Mpango wa Israeli wa upanuzi makazi ya Wayahudi huko Magharibi mwa ukingo wa mto Jordan umetajwa kuwa tishio kwa amani kati ya Israeli na Wapalestina. Waziri wa mashuri ya nchi za kigeni wa Marekani, John Kerry alisema hayo kwenye hotuba yake kuhusu nia ya serikali inayoondoka ya rais Obama ya kutaka kuwepo kwa amani kati ya Israeli na Wapalestina. Hotuba hiyo ambayo Kerry aliitoa mjini Washington imejiri siku chache tu baada ya Marekani kuwezesha baraza la Usalama la umoja wa mataifa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1979 kupitisha azimio la kutangaza upanuzi wa makazi ya Wayahudi huko magharibi mwa ukingo wa mto Jordan na mashairiki mwa mji Jerusalem kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa, baada kukataa kutumia kura yake ya turufu kupinga azimio hilo. Rais mteule wa Marekani Donald Trump ambaye awali aliihimiza Marekani kupinga azimio hilo aliwaambia wana habari kwamba Israeli haitendewi haki akisema kuna nchi nyingi duniani ambako maovu yamekithiri, lakini ni nadra kushutumiwa na baraza hilo. Hata hivyo Trump alikataa kujibu maswali kuhusu ikiwa Israeli inapasa kusitisha au kuendelea na upanuzi wa makazi hayo akisema mtazamo wake kuhusu Israeli ni bayana.