Marehemu Gachagua kuzikwa Jumatatu eneo la Mathira

Aliyekuwa gavana wa Nyeri, marehemu Nderitu Gachagua atazikwa siku ya Jumatatu ijayo nyumbani kwake Hiriga katika eneo la Mathira Magharibi. Mwili wa Gachagua uliletwa humu nchini leo asubuhi na kupokewa na jamaa zake, viongozi wa kaunti, magavana na marafiki katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Mwili huo ulisindikizwa na wanachama watatu wa baraza la magavana na jamaa zake. Akiongea katika hifadhi ya maiti ya Lee, kakaye marehemu, Rigathi Gachagua aliipongeza serikali ya kitaifa, baraza la magavana na wakenya kwa jumla kwa kuisaidia familia yake wakati huu wa majonzi. Gavana mpya wa Nyeri, balozi Samuel Wamathai na seneta Mutahi Kagwe walipongeza hasa baraza la magavana kwa kuisaidia familia hiyo tangu kifo cha Gachagua.Gachagua aliyekuwa na umri wa miaka 64 aliaga dunia wiki iliyopita baada ya kuugua kansa ya kongosho.Yeye ni gavana wa kwanza kuaga dunia akiwa yungali mamlakani.