Marehemu Gachagua azikwa nyumbani kwake Hiriga

Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nyeri marehemu James Nderitu Gachagua, alizikwa jana nyumbani kwake katika kijiji cha Hiriga, eneo bunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri katika hafla iliyounganisha utawala wa Jubilee na Upinzani. Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto, Rais mstaafu Mwai Kibaki pamoja na viongozi wa upinzani wakiongozwa na Raila Odinga, waliungana pamoja na maelfu ya waombolezaji wengine katika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Gachagua huku wakimtaja kuwa mtumishi halisi wa watu ambaye alijitolea kwa moyo wa dhati. Rais Kenyatta alikubaliana na mipinzani wake kisiasa Raila Odinga, kuhusu haja iliyopo ya kuhakikisha kwamba ugatuzi unafaidi mwananchi wa kawaida kwa mujibu wa katiba yataifa hili.