Maraga ashtumu visa vya kuhangaishwa kwa maafisa wa idara ya mahakama

Jaji mkuu David Maraga ameshtumu visa vya kuhangaishwa kwa maafisa wa idara ya mahakama kufuatia kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Urais wa tarehe 8 Agosti. Kupitia kwa tume ya huduma za idara ya mahakama Maraga alisema kwamba ikiwa lolote litatendeka kwa Ma-jaji, wafanyikazi wa Idara hiyo au familia zao, wale wanaojihusisha na matamshi ya uchochezi watawajibika binafsi. Jaji mkuu alimshtumu Inspekta-Generali wa Polisi, ambaye alisema anatarajiwa kuhakikisha usalama wa taasisi zote za serikali, lakini amekuwa akipuuza miito ya kuchukua hatua, hivyo kuhatarisha maisha na mali za maafisa wa idara ya Mahakama, na pia wahusika wa pande zote kwenye kesi. Maraga alisema inasikitisha kuona kwamba visa hivyo vinajiri wakati ambapo idara ya mahakama imeanza kusikiza rufaa 339 za kupinga matokeo ya uchaguzi kwenye mahakama mbali mbali nchini. Aligusia haswaa kesi iliyoko kwenye mahakama ya Kirinyaga, ambapoA� mlalamishi -Martha Karua, alizuiwa na waandamanaji kufika kotini wakati wa kusikizwa kwa rufaa yake. MaragaA� alisema hii ni njia moja ya kuhangaishwa kwa walalamishi na kwamba mwenendo huu haupaswi kuendelea. Jaji mkuu alisema Idara ya mahakama iko tayari kwaA� lolote katika juhudi zake za kulinda katiba na utawala wa sheria.