Maraga Aapishwa Kuwa Jaji Mkuu

Jaji mkuu mpya David Maraga alichukua rasmi wadhifa wake leo asubuhi muda mfupi baada ya kuapishwa kwenye sherehe fupi iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi. Sherehe hiyo ilishuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta , naibu wake William Ruto na spika wa bunge la kitaifa Justine Muturi miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini. Jukumu la kwanza la jaji mkuu huyo mpya litakuwa kuapisha jopo la wanachama tisa litakalowateua makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka. Akiongea muda baada ya kuapishwa, jaji mkuu Maraga aliahidi kuimarisha huduma katika idara ya mahakama kwa kukabiliana na ufisadi, kupunguza mrundiko wa kesi mahakamani na kuanzisha mfumo wa kushughulikia kesi kupitia mtandao miongoni mwa hatua nyingine..

Naye rais Uhuru Kenyatta alisema Afisi yake itashirikiana na idara ya mahakama kuhakikisha wakenya wanapokea huduma bora. Rais alitoa changamoto kwa jaji mkuu mpya kujitahidi kuharakisha uamuzi wa kesi ambazo zimekuwa mahakamani kwa muda mrefu ili kurejesha imani ya wakenya katika idara ya mahakama.