Maradhi Ya Homa Kali Ya A Na B Yazuka Katika Kaunti Ya Nakuru

Zaidi ya visa 282 vya homa kali aina ya A na B vimeripotiwa huko Nakuru katika muda wa mwezi mmoja uliopita. Akiwahutubia wanahabari katika hospitali ya Nakuru Level 5, afisa mkuu wa kaunti anayehusika na afya, Dkt. Mungai Kabii, alisema visa vya maradhi hayo vimeongezeka miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Alisema dalili za maradhi hayo ni pamoja na homa kali , kukohowa,A� shida ya kupumua, kuharisha na kutapika. Alisema maradhi hayo yanaambukizwa kupitia kukohowa na kupiga chafya. Kulingana na Dkt. Kabii matokeo ya mwanzo kutoka taasisi ya utafiti wa matibabu nchini-KEMRI yanaonyesha uwezekano wa kuzuka maradhi ya homa kali aina ya A na B. Hivyo basi Dkt. Kabii amefichua kwamba maafisa wa matibabu wamezindu wodi za kuwatenga wagonjwa wanaougua maradhi hayo katika hospitali zote za kaunti hiyo ili kushughulikia visa zaidi vya ugonjwa huo baada ya wagonjwa 39 kulazwa katika hospitali kuu ya mkoa. Kufuatia chambuko la ugonjwa huo Dkt. Kabii amesema serikali ya kaunti ya Nakuru ikishirikiana na serikali ya taifa imeandaa shughuli makhsusi ya utoaji chanjo kwa watoto wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka mitano huku akiongeza kusema kuwa wahudumu wote wa afya wamehamasishwa kuhusu ugonjwa huo.