Maoni ya Magavana Kuhusu Mswada Wa Barabara za Kaunti

Baraza la magavana litawasilisha kesi mahakamani kusimamisha halmashauri ya Mpito kuchapisha kwenye gazeti rasmi la serikali utaratibu moya wa kuorodhesha barabara. Gavana wa Taita Taveta, John Mrutu amesema hatua hiyo ni ukiukaji wa uamuzi uliotolewa na mahakama mwaka uliopita ulioagiza kuhamishwa mara moja kwa jukumu la usimamizi wa barabara za Kaunti kwa serikali za Kaunti. Mrutu pia alisema magavana hawakushauriwa wakati wa kuandaa rasimu ya mswada wa mwaka wa 2015 kuhusu barabara za humu nchini ambao uliwasilishwa katika bunge la taifa mwaka uliopita. Mrutu amesema mswada huo ulioko bungeni una utata na haujajumuisha mapendekezo ya magavana. Spika wa Seneti Kembi Gitura amesema usimamizi wa barabara za viwango vya D, E na zile ambazo hazijaorodheshwa sharti uhamishwe kwa serikali za Kaunti. Mkurugenzi mkuu wa bodi ya barabara hapa nchini Mhandisi Jacob Ruwa amesema serikali imejitolea kuhakikisha uhamishaji wa jukumu hilo kwa serikali za kaunti akiongeza kuwa kufikia sasa barabara zote zimeorodheshwa. Magavana wanataka halmashauri ya usimamizi wa barabara za sehemu za mashambani na ile inayosimamia barabara za sehemu za miji kuwa chini yao huku seneti ikipendekeza serikali ya kitaifa idumishe usimamizi wa barabara za viwango vya A, B na C.