Mandago adai kuwafuta mawaziri wazembe

Gavana mteule wa Uasin Gishu, Jackson Mandago, anasema ana mipango ya kufanyia mabadiriko baraza lake la mawaziri na kuwafuta kazi baadhi ya mawaziri wake kwa kutepetea kazini. Mandago amesema hatafanyakazi na watumishi wa umma wazembe kwani huu ndio muhula wake wa mwisho na hatakuwa na fursa nyingine ya kutetea hadhi yake. Alisema anafahamu kwamba baadhi ya wafanyikazi wa kaunti walitaka ashindwe kwenye uchaguzi mkuu tarehe 8 mwezi huu lakini akasema yuko tayari kufanya kazi na kila mmoja ambaye yuko tayari kuhudumia umma. Alikariri kujitolea kufanya kazi na mkinzani wake wa kisiasa Bundotich Buzeki, ambaye alikiri kushindwa baada ya kugombea ugavana kama mgombea huru. Hata hivyo Mandago alikanusha madai kwamba ana mipango ya kulenga jamii nyingine huko Eldoret ambazo zilionekana kumuunga mkono mpinzani wake. Mandago anatarajiwa kuapishwa tarehe 21 mwezi huu.