Manaibu wa magavana wataka sheria kuhusu urithi kurekebishwa

Mkutano wa ushauri wa manaibu wa magavana sasa unataka sheria irekebishwe ili kushughulikia swala la watakaochukua mahala pao wakijiuzulu ama kifo kikitokea. Manaibu hao wa magavana walisema mapendekezo ya dharura yanahitajika kushughulikia mwanya uliopo na kutoa utaratibu wa mwendelezo. Akiongea wakati wa kuanza kwa mkutano wao wa siku mbili huko Naivasha mwenyekiti wa mkutano huoA� Joash Maangi, alisema sheria iliyopo sasa haielezei kitakachofanyika pale nafasi itakapotokea katika ofisi ya naibu wa gavana. Kwa upande wake naibu wa Gavana wa kaunti ya Homa Bay Hamilton Orata alitoa wito wa marekebisho ya dharura ya sheria ili kushughulikia matukio ya uteuzi wa manaibu wa magavana iwapo kifo kitatokea ama watajiuzulu.

Hayo yamejiri wakati ambapo kaunti mbili zinaendesha shughuli zao bila ya manaibu wa magavana kufuatia kujiuzulu kwa naibu wa gavana wa kaunti ya Nairobi Polycarp Igathe na nafasi ya naibu wa gavana wa kaunti ya Nyeri aliyeteuliwa kuwa Gavana Mutahi Kahiga kufuatia kifo cha Dr. Wahome Gakuru ambaye alikuwa gavana wa kaunti hiyo.