Manaibu chansela wa vyuo vikuu wautaja mgomo wa wahadhiri kuwa hujuma

Manaibu chansela wa vyuo vikuu wameshutumu hatua ya wahadhiri na wahudumu wengine wa vyuo vikuu ya kugoma. Wakiongea na wanahabari baada ya mkutano katika chuo kikuu cha tekniko, manaibu chanseala hao waliwashutumu wanachama wa vyama vya UASU na KUSA kwa kukiuka makubaliano kuhusu mishahara yao wakisema tayari mashauriano yanaendelea kusuluhisha mzozo huo. Mwenyekiti wa kamati aa manaibu chansela, Profesa Francis Aduol alisema hatua hiyo haifai na wakawataka wahadhiri kurejelea mashauriano. Hata hivyo katibu mkuu wa chama cha UASU, Constantine Wasonga amewashutumu wasimamizi wa vyuo vikuu kwa kukiuka makubaliano ya kuwasilisha pendekezo lao kuhusu nyongeza ya mishahara na marupurupu mnamo tarehe 31 mwezi Mei na tarehe 1 mwezi Julai mwaka jana na mnamo miezi ya Januari na Februari mwaka huu. Ilani ya mgomo wa wahadhiri ilitolewa tarehe 21 mwezi Februari mwaka huu huku wahudumu wengine wa vyuo vikuu wakujiunga na mgomo huo Ijumaa iliyopita. Mgomo huo umeathiri shughuli za masomo kwa wanafunzi laki sita katika vyuo vikuu 31 humu nchini.