Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta Ahimiza Wakenya Waunge Mkono Miradi Mizuri

Mkewe rais Margaret Kenyatta amewahimiza Wakenya kuunga mkono miradi inayoweza kuleta mageuzi katika jamii na kulifanya taifa hili mahali bora pa kuishi kwa Wakenya wote.

Akiongea jana jioni kwenye hafla ya kumbukumbu ya marehemu mwanaharakati wa mazingira Profesa Wangari Mathai kwenye makavazi ya kitaifa, Bi Kenyatta alisema ulimwengu unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji juhudi za watu wenye ukakamavu ili kuhakikisha maisha bora ya vizazi vijavyo.

Bi Kenyatta aliwahimiza Wakenya kuimarisha maadili na matumanini miongoni mwa vijana.

Alimuenzi marehemu Profesa Wangari Mathai kwa kuwa mmoja wa watu waliodhihirisha ujasiri ili kuboresha maisha ya Wakenya na kuleta mageuzi katika jamii. Alisema juhudi za Profesa Mathai za kuhifadhi mazingira zilileta mabadiliko makubwa katika mazingira ya taifa hili.

Hafla hiyo pia ilishuhudia kubuniwa kwa kituo kinachozingatia uhifadhi wa mazingira kwa jina Wangari Maathai House kitakachotumiwa kama kitovu cha kuleta mabadiliko ulimwenguni.