Mama wa taifa awasili London kwa mkutano kuhusu biashara haramu ya wanyama pori

Mama wa taifa Margaret Kenyatta amewasili nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa nne wa London kuhusu biashara haramu ya wanyama pori.

Mama wa taifa ambaye ni mdhamini wa juhudi za kuzuia uwindaji ndovu anaongoza ujumbe wa Kenya kwenye mkutano huo.  Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, ataufungua mkutano huo wa siku mbili utakaofanyika huko Battersea Evolution, London.

Mkutano huo ulioandaliwa na serikali ya Uingereza utawaleta pamoja viongozi wa ulimwengu kujadili mikakati itakayoimarisha juhudi za kitaifa na kimataifa ili kumaliza biashara haramu ya wanyama pori na kulinda spishi muhimu za wanyama pori wanaotishiwa kuangamia. Mkutano huo utawaleta pamoja wajumbe kutoka nchi 75.