Malumbano kati TSC, KNUT hatari kwa maafikiano

 Malumbano kati ya tume ya kuwaajiri waalimu-TSC na chama cha taifa cha waalimu-KNUT huenda yakahatarisha maafikiano kati ya taasisi hizo mbili ambayo yaliwezesha kuahirishwa kwa mgomo wa waalimu uliopangiwa tarehe mosi mwezi huu.

Chama cha KNUT kinalaumu tume ya TSC kwa kukiuka maazimio yalioafikiwa kwenye mkutano wa mashauriano tarehe 23 mwezi uliopita ambao ulikubaliana kusitisha zoezi la kuwahamisha waalimu na lile la kutathmini utendakazi wao. Katibu mkuu wa chama cha KNUT, Wilson Sossion, alisema hata baada ya tume ya TSC kukubali  kusitisha sera za kuwahamisha na kutathmini utendakazi wa waalimu miongoni mwa masuala mengine, tume hiyo imewachukulia hatua waalimu wanaodaiwa kukiuka maagizo kuhusu sera hizo.

Hata hivyo tume ya kuwaajiri waalimu na chama cha KNUT zimekubaliana kuandaa mkutano wa siku tano kuanzia tarehe 30 mwezi huu, mkutano ambao maafisa wa chama hicho wanasema utaamua mwelekeo wa kuchukuliwa kuhusiana na mgomo wa waalimu ulioahirishwa. Chama cha KNUT pia kimehimiza kuondolewa barua za kuwachukulia waalimu hatua za kinidhamu huko Masaba kaunti ya Nyamira na tume ya TSC kwa kuchoma fomu za kutathmini utendakazi wao.