Majeshi Ya Kenya Yawaua Zaidi Ya Wafuasi 60 Wa Al-Shabaab

Huku vita dhidi ya ugaidi vikiimarishwa majeshi ya Kenya yamewaua zaidi ya wafuasi 60 wa al-Shabaab kwenye kambi zao karibu na mji wa Beled-Hawo nchini Somalia. Duru za kijeshi zimesema kuwa magaidi hao waliuawa walipokuwa wamejificha kwenye vijiji kufuatia kuimarishwa kwa operesheni za kijeshi zilizojumuisha majeshi ya Kenya, ujumbe wa Afrika nchini Somalia na jeshi la kitaifa la Somalia. Duru hizo zilisema kuwa wanamgambo hao wamekuwa wakishambulia vituo vya kijeshi kwa kurusha guruneti kutoka kwenye vijiji hivyo. Mashambulizi ya angani yaliyotekelezwa na majeshi ya Kenya yalikumba vituo sita yakiwemo malori na magari aina ya pickup yaliyokuwa na bunduki. Majeshi ya Kenya yameimarisha operesheni kufuatia shambulizi lililotibuka lililolenga kambi ya jeshi la Kenya la Mangai huko Baure, kaunti ya Lamu. Kwenye shambulizi hilo lililotekelezwa siku ya Jumanne wanajeshi hao waliwaua wanamgambo wanne wa kundi hilo wanaohusishwa na kikundi cha Jaysh Ayman kinachotekeleza vitendo vyake kutoka msitu wa Boni.