Majaji wa mahakama ya juu wanajadili na kuandika uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa na NASA

Majaji wa mahakama ya juu wamekwenda faraghani kujadili na kuandika uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa na muungano wa NASA kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka huu. Hii ni baada ya mawakili wa pande husika pamoja na mwanasheria mkuu profesa Githu Muigai na mawakili wa chama cha wanasheria ambao walijumuishwa kama marafiki wa mahakama kutoa mawasilisho yao Jumanne jioni. Jaji mkuu David Maraga aliwahakikishia Wakenya kuwa mahakama hiyo itakamilisha shughuli hiyo kwa muda ufaao na kutoa uamuzi wao Ijumaa hii. Hata hivyo hakubainisha wakati wa kutoa uamuzi huo huku akisema msajili wa mahakama ya juu atawasiliana na pande husika kuhusu suala hilo. Jaji Maraga aliwashukuru mawakili kwenye kesi hiyo kwa kuendesha shughuli hiyo kwa ustaarabu na akawahimiza kudumisha moyo huo. Maoni yake yalipokewa vyema na mawakili wa pande husika waliowasifu majaji wa mahakama hiyo kwa kujitolea kwao kusikiza kesi hiyo. Rufaa hiyo iliwasilishwa na mgombeaji wa muungano wa NASA kwenye uchaguzi wa urais wa mwezi huu, Raila Odinga na mgombeaji mwenza Kalonzo Musyoka. Wawili hao wakiandamana na viongozi wengine wa muungano huo walihudhuria vikao vya mahakama hiyo kwa siku mbili. Mawakili wa muungano huo waliongozwa na James Orengo ilhali wale wa tume ya IEBC na mwenyekiti wake Wafula Chebukati waliongozwa na Paul Muite. Mawakili wa rais Uhuru Kenyatta waliongozwa na Fred Ngatia. Macho ya Wakenya sasa yameelekezwa kwenye uamuzi utakaotolewa na majaji wa mahakama ya juu wakiongozwa na jaji mkuu David Maraga, naibu jaji mkuu Philomena Mwilu, Isaac Lenaola, Njoki Ndunga��u, Smokin Wanjala, Jackton Boma Ojuang na Mohammed Ibrahim ambaye hata hivyo aliripotiwa kuugua jana.