Mahakama yahurusu NASA kupata data kutoka kitovu cha mtandao wa IEBC

Mahakama ya juu imeagiza tume ya IEBC kuruhusu muungano wa NASA kupata data kutoka kitovu cha mtandao wake. A�Aidha mahakama hiyo imeagiza tume hiyo kuwasilisha fomu 34A, 34B na 34C zilizotumiwa kujumlisha kura za urais kutoka vituo vya kupigia kura na maeneo bunge. Hata hivyo, mahakama hiyo ilikatalia mbali ombi la muungano wa NASA la kuruhusiwa kupata data kutoka mfumo wa kubainisha wapiga kura kwani kampuni husika haijajumuishwa kwenye rufaa hiyo. Kwenye uamuzi uliosomwa na jaji Isaac Lenaola, mahakama hiyo iliagiza tume ya IEBC kuwasilisha stakabadhi za kubainisha mahali ambapo kila kifaa kilichotumiwa kupeperusha matokeo ya uchaguzi kilikuwa wakati wa uchaguzi mkuu kwa mawakili wa muunagno wa NASA na rais Uhuru Kenyatta. Aidha tume hiyo inapasa kuwasilisha sera yake kuhusu mikakati ya kukabiliana na changamoto za ki-mtandao, stakabadhi za kubainisha ni nani walitumia vifaa hivyo na wasimamizi ambao wamekuwa wakishughulikia vifaa hivyo kuanzia tarehe-5 mwezi huu hadi kufikia sasa. Mahakama iliagiza kuwe na uhasibu na uchunguzi wa kina wa mfumo wa uchaguzi chini ya usimamizi wa msajili wa mahakama ya juu. Aidha mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya maawsiliano wa idara ya mahakama na wataalamu wawili huru watashiriki katika shughuli hiyo na kuwasilisha ripoti zao.