Mahakama Yahairisha Hukumu Ya Madaktari Wanaogoma

Hukumu iliyokuwa ikisubiriwa kutekelezwa dhidi ya maafisa wa chama cha madakati imesitishwa. Maafisa wa chama hicho wakiongozwa na katibu mkuu wao Ouma Oluga walipaswa kuanza kutumikia kifungo cha mwezi mmoja gerezani hivi leo baada ya kushindwa kukomesha mgomo wa kitaifa wa madaktari jinsi walivyoagizwa na mahakama. Hata hivyo walishawishi mahakama ya kushughulikia mizozo ya ajira kuahirisha hukumu hiyo kwa siku tano. Katika uamuzi wake kuhusu ombi la madaktari la kutaka muda huo uongezwe kwa wiki mbili, jaji Helen Wasilwa aliwapa siku tano zaidi kukomesha mgomo huo la sivyo watafungwa jela. Jaji huyo alisema siku tano zaidi zitatoa fursa kwa chama hicho cha madaktari kuendelea na mazungumzo na serikali na kutia saini mkataba. Alisema uamuzi wake ulitokana na kujali maslahi ya umma.