Mahakama ya rufani yaamua Al Ghurair iendelee na uchapishaji karatasi za kura za urais

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa inaweza kuendelea na zabuni ya uchapishaji karatasi za uchaguzi wa urais iliyotolewa kwa kampuni ya uchapishaji ya Al-ghurair. Hiyo ni baada ya mahakama ya rufani kubadili uamuzi wa awali wa mahakama kuu ulioiagiza IEBC kutangaza upya zabuni hiyo ya uchapishaji karatasi za uchaguzi. Katika uamuzi wa pamoja jopo hilo la majaji :- Erastus Githinji, Roselyn Nambuye, Alnashir Visram, Professor James Ouko na Jamila Mohamed liliamua kwamba uamuzi wa mahakama kuu haukujali muda uliosalia kikatiba ambapo uchaguzi mkuu ukiwemo uchaguzi wa Urais unapaswa kufanyika. Pia mahakama hiyo iliamua kwamba ushiriki wa umma kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama kuu wa kubatilisha zabuni hiyo ya Alghurai haukuwa wa lazima wakati wa utoaji zabuni moja kwa mojaA� isipokuwa matukio maalum. Jopo hilo liliamua kwamba uamuzi wa mahakama kuu haukufikiria hatima ya mamilioni ya wakenya katika kutekeleza haki zao za kuwa na uchaguzi huru, wa haki na wa kawaida kwa kuzingatia hitaji la kikatiba. IEBC ilipinga uhalali wa uamuzi wa mahakama hiyo wa kutenganisha karatasi za uchaguzi wa urais na nyadhifa nyinginezo kwenye zabuni iliyopewa kampuni ya Al Ghurair, ikisema uamuzi huo si halali.