Mahakama ya Rufani Kisumu yadumisha ushindi wa Gavana Obado

Mahakama ya rufani mjini Kisumu imedumisha kuchaguliwa kwa gavana wa Migori  Okoth Obado. Mahakama hiyo ilikatalia mbali rufaa iliyowasilishwa na mpinzani wake Ochillo Ayacko ambaye alikuwa akipinga uamuzi wa mahakama kuu. Kwenye uamuzi huo uliosomwa na jaji Steven Gatembu, majaji wa mahakama ya rufani walisema Ochillo Ayacko alishindwa kuthibitisha kuwa uchaguzi huo haukuandaliwa kuambatana na kanuni za sheria. Majaji hao walisema mahakama kuu haikukosea kwa kutupilia mbali rufaa hiyo. Hata hivyo mahakama hiyo imepunguza gharama ya kesi hiyo kutoka shilingi milioni sita hadi milioni tatu.

Wiki moja iliyopita  Ayacko aliondoa rufaa yake mahakamani baada ya kuafikia makubaliano na  Obado lakini mahakama ya rufani iliamua kutoa uamuzi kwa sababu kesi hiyo ilikuwa imesikilizwa tayari. Ayacko, kupitia wakili wake  Nyamori Nyasyimi alifika kwenye mahakama hiyo akisema jaji wa mahakama kuu Hillary Chemitei alimnyima haki kwa kufutilia mbali maombi na ushahidi wake kwenye rufaa hiyo.