Mahakama ya Niger imemhukumu kiongozi mkuu wa upinzani kwa ulanguzi wa watoto

Mahakama moja nchini Niger imemhukumu kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Hama Amadou kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa kosa la ulanguzi wa watoto. Amadou alimpinga rais Mahamadou Issoufou katika uchaguzi wa mwezi Machi nchini humo. Kwa sasa yuko uhamishoni nchini Ufaransa na alihukumiwa kifungo hicho bila yeye mwenyewe kuwa mahakamani. Mawakili wake hawakuwa mahakamani kwa vile walisusia kikao hicho ili kulalamikia kesi hiyo ambayo wanadai kuwa haifai. Amadou anadaiwa kukanusha mashtaka dhidi yake. Inasemekana kuwa alikuwa akinufaika kwa kununua watoto wanaozaliwa kutoka taifa jirani la Nigeria. A�Inadaiwa kuwa yeye na mkewe pamoja na watu wengine walihusika na njama hiyo. Mawakili wa upande wa utetezi walidai kuwa kesi dhidi yake ilikuwa inachochewa kisiasa na inapaswa kuahirishwa ili kutoa muda wa stakabadhi zinazohusiana na kesi hiyo kuwasilishwa kwake nchini Ufaransa. Hata hivyo ombi lao lilikataliwa na jaji anayesimamia kesi hiyo.