Mahakama Ya Juu Yasimamisha Hatua Ya Kubinafsisha Kampuni 5 Za Sukari

Mahakama ya juu imesimamisha hatua ya kubinafsisha kampuni 5 za utayarishaji sukari katika eneo la mgharibi. Akitoa agizo hilo, Jaji Weldon Korir wa mahakama kuu aliiagiza tume inayosimamia shughuli ya ubinafsishaji kutoendelea na uuzaji huo hadi pale itakaposhauriana na wadau na kutatua maswala tata yaliyopo. Kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa siku ya jumatatu, seneta wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o na mbunge wa Gem, Jakoyo Midiwo waliikosoa tume hiyo kwa kutozingatia kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria za ubinafsishaji. Walidai kwamba muundo wa tume hiyo ya ubinafsishaji kwa sasa haufai. A�Aidha walidai kwamba wadau hasa wakuzaji miwa hawajaarifiwa kuhusu shughuli hiyo. Kwenye stakabadhi zao za mahakama, viongozi hao wawili walidai kwamba shughuli ya kubinafsisha kampuni za sukari za Miwani na Muhoroni zilizo chini ya urasimu, pamoja na zile za Nzoia, Chemelil na South Nyanza, ni ubatili.