Mahakama ya Juu kuamua kuhusu matokeo ya urais Ijumaa

Majaji wa mahakama ya juu wamekwenda faraghani kujadii na kuandika uamuzi wa rufaa iliyowasilishwa na muungano wa NASA kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka huu. Hii ni baada ya mawakili wa pande husika pamoja na mwanasheria mkuu profesa Githu Muigai na mawakili wa chama cha wanasheria ambao walijumuishwa kama marafiki wa mahakama kutoa mawasilisho yao jana jioni. Jaji mkuu David Maraga aliwahakikishia Wakenya kuwa mahakama hiyo itakamilisha shughuli hiyo kwa muda ufaao na kutoa uamuzi wao Ijumaa hii. Hata hivyo hakubainisha wakati wa kutoa uamuzi huo huku akisema msajili wa mahakama ya juu atawailiana na pande husika kuhusu suala hilo. Jaji Maraga aliwashukuru mawakili kwenye kesi hiyo kwa kuendesha shughuli hiyo kwa ustaarabu na akawahimiza kuendelea vivyo hivyo.