Mahakama Kuu Yasikiliza Kesi Inayowakabili Wabunge Wanane

Mahakama kuu kwa sasa inasikiliza kesi inayowakabili wabunge wanane wanaotuhumiwa kwa kutoa matamshi ya chuki ambao wanataka kuachiliwa huru kwa dhamana baada ya kuzuiliwa korokoroni katika muda wa siku nne. Wabunge hao walikuwa wakizuiliwa katika korokoro za vituo vya polisi vya Pangani na Muthaiga kuanzia Jumanne baada ya kukamatwa kwa madai ya kutoa matamshi ya chuki . Wabunge hao kutoka mirengo ya Jubilee na CORD walisafirishwa kwa magari ya polisi hadi katika mahakama ya Milimani leo mwendo wa saa 12 kasorobo alfajiri . Wabunge Moses Kuria wa Gatundu Kusini , Kimani Ngunjiri wa Bahati, Ferdinand Waititu wa Kabete , Junet Mohamed wa Suna Mashariki , Timothy Bosire wa Kitutu Masaba, Aisha Jumwa ambaye ni mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kilifi , Florence Mutua, ambaye ni mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Busia na seneta Johnstone Muthama wa kaunti ya Machakos wamefikishwa mbele ya jaji Daniel Ogembo . Hapo jana muungano wa CORD ulitishia kurejelea maandamano ya barabarani siku ya Jumatatu iwapo wabunge wa mrengo huo hawataachiliwa huru bila masharti katika muda wa saa 24 . Kiongozi wa CORD Raila Odinga ameshtumu serikali kwa kukiuka haki za wabunge waliozuiliwa kwa kuwakataza kupata mawakili wanaotaka , kuwanyima chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Rais Uhuru Kenyatta akiongea mjini Brussels, Ubeljiji amesema serikali yake haitavumilia visa vya matamshi ya chuki au uchochezi wa ghasia.