Mahakama kuu yadumisha ushindi wa gavana Sospeter Ojamong

Zilikuwa shangwe na nderemo katika kaunti ya Busia huku wakazi wakisherehekea uamuzi wa mahakama kuu wa kudumisha ushindi wa gavana wa kaunti hiyo Sospeter Ojamong. Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo iliyowasilishwa na mpiga kura Peter Odima kutoka eneo bunge la Nambale ilitupiliwa mbali na mahakama kwa kutokuwa na ushahidi wa kutosha. Odima alikuwa mkuu wa kampeini za aliyekuwa mbunge wa Funyula Paul Otuoma ambaye aligombea kiti hicho cha ugavana na kuibuka wa pili. Ojamong aligombea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha ODM. Jaji Kiarie Waweru Kiarie alisema baada ya kuchunguza ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili , ilibainika kuwa uchaguzi huo ulifanywa kulingana na katiba ya Kenya. Jaji Waweru alimuagiza Odima kulipa shilling million 12 kama gharama za kesi hiyo. Kila mshtakiwa atapokea shilling million nne. Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa ni pamoja na Ojamong ,tume ya IEBC na afisa aliye-simamia uchaguzi huo, Fredrick Apopa.