Mahakama Kuu Yadinda Kukomesha Kikao Maalum Cha Bunge La Kitaifa

Mahakama kuu jana ilikataa kutoa maagizo ya kulizuia bunge la kitaifa kuandaa kikao maalum kuhusiana na sheria za kiuchaguzi. Kwenye uamuzi wake, jaji George Odunga alisema kuwa mahakama haina mamlaka yoyote ya kuingilia shughuli ya kubuni sheria ila tu inaweza kushughulikia matokeo yake. Justice Odunga alisema kwa sasa mahakama haingeweza kubainisha iwapo marekebisho hayo yangepitishwa. Hata hivyo Justice Odunga aliwaambia wapinzani kwamba wanaweza kupinga marekebisho hayo mahakamani iwapo sheria zilizopitishwa zinakiuka katiba. Muungano wa CORD kupitia kwa mawakili wao Seneta James Orengo na Paul Mwangi waliwasilisha kesi mahakamani Jumatano usiku kupinga kikao maalum cha bunge cha leo. Muungano huo ulisema kuwa kikao ambacho kilirekebisha sheria za kiuchaguzi leo asubuhi ni kinyume cha sheria na wakatafuta mwingilio wa dharura wa mahakama.