Mahakama Kuu Yaagiza Serikali Kurejesha Walinzi Wa Mbunge Timothy Bosire

Mahakama kuu imeiagiza serikali kuwarejesha walinzi wa mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire hadi pale kesi aliyowasilisha mahakamani itakaposikizwa na kuamuliwa. Akitoa maagizo hayo jaji Isaac Lenaola alisema kuondolewa kwa walinzi wa mbunge huyo kunaibua masuala ya ubaguzi. Kesi hiyo itasikizwa tarehe 27 mwezi huu. Bosire, amemshtaki waziri wa usalama wa taifa Joseph Nkaiserry na inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinett kufuatia hatua ya kuondolewa walinzi wake. Bosire anadai walinzi wake waliondolewa baada ya yeye kujikokota kusimama kuwaenzi wanajeshi wa vikosi vya ulinzi waliouawa nchini Somalia wakati wa hotuba ya rais Uhuru Kenyatta kuhusu hali ya taifa tarehe 31 mwezi uliopita. Alisema uamuzi wa kuwaondoa walinzi wake ulifanywa bila mashauriano hatua ambayo ni ukiukaji sheria. Mbunge huyo anadai kuwa hakusimama kwani hakutaka kufurahisha umma huku akipuuza masaibu yanayowakumba wanajeshi wa nchi hii huko nchini Somalia.