Mahakama kuamua kesi dhidi ya uchaguzi Jumatatu

Mahakama ya juu mnamo Jumatatu wiki ijayo itaamua ikiwa itadumisha kuchaguliwa tena kwa rais Uhuru Kenyatta ama kuagiza uchaguzi kufanywa upya katika muda wa siku 60. Mwanasheria mkuu Githu Muigai hata hivyo ametahadharisha majaji ya mahakama ya juu dhidi ya kutangua marudio ya uchaguzi wa urais akisema uamuzi kama huo utawazawadia tu wale wanaohujumu katiba. Akiongea alipotoa mawasilisho yake katika mahakama ya juu kama mtu mwenye maslahi alisema rufaa za uchaguzi zinazaonuia kutangua ushindi wa rais Uhuru Kenyatta kwenye marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi Oktoba, Profesa Muigai alisema rufaa hizo hazijabainisha ushahidi wa kutosha na zinahusu tu msururu wa malalamishi.

Kwa upande wao mawakili wa rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na wakili Fred Ngatia walikosoa ushahidi uliowasilishwa na walalamishi wakiwahimiza majaji wa mahakama ya juu kutupilia mbali kwa gharama rufaa hizo zilizo mbele yao kwa misingi kwamba yaliowasilishwa na walalmishi hayawezi kubainishwa.Majaji sasa wameenda kuchunguza hati zilizowasilishwa mahakamani na mahakama ya juu itatoa uamuzi wake Jumatatu wiki ijayo. Jaji mkuu David Maraga hata hivyo hakusema wakati ambapo uamuzi huo utatolewa.