Magufuli atarajiwa kuwasili nchini kenya kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuandaa mazungumzo ya pande mbili na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ambaye atawasili hapa nchini leo kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Hiyo itakuwa ziara yake ya kwanza hapa nchini tangu alipochaguliwa kuwa rais mwezi Oktoba mwaka 2015. Marais hao wawili watajadili maswala yanayohusu nchi hizi mbili kama vile vibali vya kazi na viwango vya juu vya karo za vyuo vikuu zinazotozwa wakenya , kuondolewa kwa vikwazo vya biashara kati ya nchi hizi mbili , tume ya pamoja ya Tanzania kuhusu ushirikiano, na azma ya Amina Mohammed ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika.

Kwenye taarifa msemaji wa ikulu Manoah Esipisu amesema rais Magufuli atafungua rasmi barabara kuu ya kusini mwa jiji la Nairobi . Manoah pia ametangaza kuwa kongamano la ikulu kuhusu teknolojia ya habari na mawasiliano ambalo lilipangiwa kuandaliwa leo limeahirishwa hadi tarehe 7 Novemba.

Cha muhimu ni kwamba mawaziri kutoka mashirika ya COMESA, EAC na SADC wanaandaa mkutano jijini Nairobi kujadili swala la kubuniwa kwa eneo la soko huru ambalo litaashiria hatua kubwa katika utangamano wa bara la Afrika. Waziri wa viwanda Adan Mohammed anaongoza ujumbe wa Kenya kwenye mkutano huo.

A�