Magavana walalamika kuhusu kuchelewa katika usambazaji wa fedha kwa serikali za kaunti

Baraza la magavana limelalamikia hatua ya wizara ya fedha ya  kuchelewesha  kila mara kusambaza  fedha  kwa  serikali za kaunti  na kusema kutojitolea kikamilifu kwa serikali ya kitaifa kuafikia malengo ya ugatuzi. Mwenyekiti wa baraza hilo Josphat Nanok, amesema  kucheleweshwa huko kwa fedha kumelemaza shughuli za serikali za kaunti huku  zikilazimika kupunguza miradi zinazofadhili au hata kuzisimamisha. Nanok alisema kutolewa kwa fedha wakati usiofaa  ni kikwazo katika utekelezaji wa ugatuzi  na akaongeza kuwa ili kuafikia  ustawi  wa kina viwago vyote vya serikali  lazima virishikiane  na kufanya kazi kwa uwazi. Nanok ambaye pia ni Gavana wa  Kaunti ya  Turkana  alisema  hayo  mjini  Nyeri  wakati wa kufunguliwa kwa warsha ya kila mwaka kuhusu tume za kikatiba na afisi huru.Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga, alisema  utekelezaji wa katiba mpya una changamoto ambazo zinastahili kushughulikiwa ili hatua ipigwe. Alisema sheria ya mpito inastahili kurekebishwa. Alitoa mfano wa  sheria inayomzuia kuteua naibu wake kufuatia kifo cha mtangulizi wake Wahome Gakuru kuwa kikwazo kwa utendaji kazi.