Magavana Hatimaye Kukubaliana Juu Ya Kiasi Cha Ushuru

Magavana sasa wanasema wako tayari kukubali mgao wa asilimia 35 wa ushuru badala ya asilimia 45 waliokuwa wakiitisha hapo awali.Akiongea wakati wa mkutano wa baraza la kiuchumi na bajeti la serikali ya kitaifa na zile za Kaunti uliondaliwa katika afisi ya naibu wa rais William Ruto iliyoko Karen hapa mjini Nairobi, mwenyekiti wa baraza la magavana Peter Munya alisema wako tayari kukubali kiasi hicho cha mgao wa ushuru wa kitaifa. Munya alisema ipo haya ya maafikiano kuhusu ufadhili wa baadhi ya majukumu yaliyogatuliwa na akataka serikali za kaunti kushirikiana na ile ya taifa ili kuimarisha utoaji huduma.Naye waziri wa fedha Henry Rotich alisema serikali ya taifa itaheshimu vipengee vya katiba kuhusu mgao wa rasilimali za kitaifa.Mkutano huo ulijadili mgao wa ushuru wa kitaifa wakati wa kipindi kijacho cha matumizi ya pesa za serikali, rasimu ya sera kuhusu bajeti na kuhamishwa kwa majukumu yaliyogatuliwa.