Magaidi wasakwa baada ya kutekeleza shambulizi Lamu

Vikosi vya ulinzi hapa nchini vinawasaka wanamgambo wa kiislamu ambao wanaaminika kuhusika na shambulizi la kujilipuzi cha kujitengenezea huko Kiunga katika kaunti ya Lamu ambako watu wanane waliuawa miongoni mwao maafisa saba wa polisi wa utawala na raia mmoja. Shambulizi hilo la siku ya Jumatano linafikisha idadi ya polisi waliouawa wakiwa kazini kuwa 20 katika muda wa wiki moja. Wiki iliyopita polisi 13 wa utawala waliuawa kwenye mashambulizi katika kaunti za Garissa na Mandera ambako gavana Ali Roba aliponea chupu chupu ambapo walinzi wake watano walifariki. Inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinett alitangaza mapema wiki hii kwamba kundi la Al-Shabaab limekuwa likiimarisha mashambulizi hapa nchini baada ya serikali ya Somalia kutangaza mashambulizi mapya dhidi ya kundi hilo la kigaidi. Kundi la Al-shabbab limebadili mbinu zake na kuazimia kutumia vilipuzi vya kujitengenezea katika baadhi ya sehemu za pwani na mkoa wa kaskazini mashariki kulingana na polisi. Haya yanajiri huku duru zikidokeza kwamba wanamgambo wamewateka nyara waalimu wawili huko Fafi kaunti ya Garissa kwenye kisa kingine tofauti kilichojiri Jumatano usiku.