Maelfu Ya Waisilamu Waadhimisha Idd-Ul-Adha

Maelfu ya waumini wa kiislamu jana walifurika katika maeneo tofauti hapa nchini kwa sala za idd-Ul-Adha kuadhimisha mwisho wa hija ya kwenda mjini Mecca nchini Saudi Arabia. Jijini Nairobi waumini wa kiislamu walikongamana katika klabu ya Sir Ali Muslim ambako kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa Aden Duale aliwaongoza viongozi wengine wa kiislamu kushtumu kisa cha hivi majuzi huko Mombasa ambako wanawake watatu waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa jaribio la shambulizi la kigaidi lililotibuka katika kituo cha polisi cha central.

Huko Mombasa sala ziliandaliwa huku viongozi wa kiislamu wakiwahimiza waislamu kudumisha amani na kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kukabiliana na itikadi kali za kidini.

Shirika lisilokuwa la serikali la Kuwait kwa jina Direct Aid International,A�limetoa mifugo 2,500 ili kuchinjwa wakati wa sherehe za kiislamu za Idd-Ul-Adha. Wanyama hao ambao ni ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi walisambazwa kwa jamii maskini katika maeneo kame bila ubaguzi kwa mujibu wa mkurugenzi wa shirika hilo, dakta Esmail Hassan. Mkurugenzi huyo alimpongeza rais Uhuru Kenyatta kwa kutangaza sherehe za Idd-Ul-Adha kuwa siku ya mapumziko.A� Wakati wa sherehe hizo ambazo pia zinajulikana kama sherehe za kutoa kafara, waislamu huhitajika kumchinja mnyama kwa ukumbusho wa nabii Abraham aliyejitolea kumtoa mwanawe kafara kama hatua ya utiifu kwa amri ya Allah.