Madaktari waagizwa kurudi kazini iwapo wanataka serikali kuendeleza mashauriano

Madaktari wameagizwa kurejea kazini iwapo wanataka serikali kuendelea kushauriana nao. Hatibu wa Ikulu, Manoah Esipisu, jana alikariri msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba Madaktari sharti wafahamu serikali haitavumilia mchezo mwingine wowote kutoka kwa wafanyikazi walio kwenye mgomo haramu. Esipisu alisema Rais anafahamu juu ya taarifa kutoka kwa Chama cha Madaktari ambayo inaomba muda zaidi wa mashauriano, lakiniA� Rais Kenyatta amebainisha wazi msimamo wake.Wakati huo huo kundi la upatanishi linalonuia kukomesha mgomo unaoendelea wa madaktari linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya mwisho mbele ya mahakama ya rufani hapo kesho. Kundi hilo linaloongozwa na baraza la dini mbalimbali limefanikisha kuafikiwa kwa mkataba kuhusiana na maswala mbalimbali tata isipokuwa njia za kutia saini hati hizo tatu. Majaji Hannah Okwengu, Martha Koome na Sankale Ole Kantai wa mahakama ya rufani juma lililopita waliagiza kwamba swala hilo litajwe siku ya Jumatatu ili kuandikisha taarifa, baadhi ya kaunti tayari zimeanza kutekeleza agizo la kuwafuta kazi madaktari ambao hawajarejea kazini. Katika kaunti ya Kiambu, gavana William Kabogo, amesema tayari serikali yake imewafuta kazi madaktari wanaogoma na anawatarajia madaktari kutoka India katika muda wa juma moja lijalo.