Madaktari kulegeza msimamo wao kuhusiana na mgomo

Madaktari wako tayari kulegeza msimamo wao na kuafikia makubaliano iwapo serikali itafanya vivyo hivyo. Wakiongea walipofika mbele ya kamati ya seneti kuhusu afya, maafisa wa chama cha madaktari na wataalamu wa meno KMPDU waliieleza kamati hiyo kwamba wamejaribu kuafikia makubaliano na serikali bila mafanikio. Katibu mkuu wa chama cha KMPDU daktari Ouma Oluga aliilaumu serikali kwa kutoshughulikia ipasavyo mgomo wa madaktari ambao umeingia siku yake ya 65, akisema madaktari wanavunjika moyo. Daktari Oluga alisema baadhi ya vipengele vinavyozua utata katika mkataba wa pamoja ni muhimu kwani vitasaidia kulainisha sekta hiyo hapa nchini. Katibu huyo mkuu wa KMPDU alisema upataji mafunzo, uajiri na mazingira duni ya kazi ni mojawapo wa nyanja wanazotaka zichunguzwe na serikali.Mwenyekiti wa kamati ya seneti kuhusu afya, seneta Wilfred Machage alikariri kwamba mkataba huo ulioafikiwa mwaka 2013 sio halali kwani ulitiwa saini na katibu katika wizara ambaye alikuwa ameshushwa cheo siku mbili zilizotangulia. Katibu wa zamani Mark Bor alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya serikali.A� Mgomo huo umesababisha jaji Hellen Wasilwa kuwahukumu maafisa wa chama cha KMPDU kifungo cha mwezi mmoja gerezani kwa kukiuka agizo la mahakama la kusitisha mgomo. Hatua ya katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikaziA� COTU, Francis Atwoli ya kuingilia kati wiki iliyopita, imeisababisha mahakama kuwaongeza muda wa siku 7 zaidi ili kuafikia makubaliano.