Madai Ya Uchochezi Nchini Burundi Yahusishwa Na Maafisa wa Rwanda

Marekani imeelezea wasiwasi kuhusiana na ripoti kuwa kuna baadhi ya maafisa nchini Rwanda ambao wanadaiwa kuhusika na uchochezi wa ghasia nchini Burundi. Rwanda imedaiwa kuwa na wakimbizi waliojihami na waliopewa mafunzo kusaidia upinzani kupigana na serikali nchini Burundi. Serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai. Burundi imekuwa ikikabiliwa na ghasia zilizosababishwa na hatua ya rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza ya kuamua kuwania hatamu ya tatu ya urais nchini humo. Zaidi ya watu 400 wamefariki katika ghasia hizo huku wengine wapatao elfu 240 wakisemekana kutoroka taifa hilo.