Mabalozi waliopendekezwa wasailiwa huku Serem akikanusha kulenga wabunge katika utathmini wa mishahara

Balozi wa Kenya aliyependekezwa kuliwakilisha taifa hili nchini Uchina Sarah Serem amekanusha madai ya wabunge kwamba shughuli ya kuwianisha mishahara ya watumishi wa umma iliwalenga zaidi wabunge. Akiongea alipofika mbele ya kamati ya bunge la taifa kuhusu ulinzi na mashauri ya kigeni  mwenyekiti huyo wa  zamani wa tume ya mishahara na marupurupu SRC alitetea wadhifa wake wa zamani akisema utathmini wa kazi na mishahara ulitokana na haja ya kupunguza gharama kubwa ya mishahara inayoathiri uchumi wa nchi.

Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Upelelezi Ndegwa Muhoro aliyependekezwa kuwa balozi wa Kenya nchini Malaysia alikanusha taarifa iliyowasilishwa na wakili Ahmednassir Abdullahi ambaye aliwataka wabunge kumkataa Ndegwa kwamba hafai. Muhoro atahitajika kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Malaysia na Kenya.

Msemaji wa zamani wa Ikulu Manoah Esipisu aliyependekezwa kuwa balozi wa Kenya nchini Uingereza pia alikuwa na fursa ya kuelezea ni kwa nini anafaa kuteuliwa kwa wadhifa huo. Mbunge wa Belgut Nelson Koech alimhoji msemaji huyo wa zamani wa Ikulu akimshtumu kwa kutumia ofisi yake ya zamani kutafuta pesa kwa shughuli za rais ambazo tayari zimetengewa bajeti.

Wengine waliopendekezwa kuwa mabalozi ni pamoja na mbunge wa zamani wa Kasipul Kabondo Paddy Ahenda na luteni jenerali mstaafu Samuel Thuita.