Maandalizi ya mashindano ya tenisi ya mezani Barani Afrika katika uwanja wa kimataifa Moi Kasarani yamekamilika

 Maandalizi ya mashindano ya tenisi ya mezani Barani Afrika  yatakayoanza leo katika ukumbi wa uwanja wa kimataifa Moi Kasarani,yamekamilika. Mashindano hayo ya siku tatu ambayo pia yatatumiwa kufuzu kwa mashindano ya dunia mwaka ujao, yamewavutia wachezaji kutoka mataifa thelathini. Katika mashindano hayo, Kenya  itawakilishwa na Sejal Thakkar na  Brian Mutua. Wachezaji hao wanawania nafasi mbili zilizotengewa Bara Afrika katika mashindano ya dunia mwaka huu. Akinadada kumi na sita, akiwamo bingwa mtetezi  Dina Meshref  wa Misri watashiriki katika kinyang’anyiro hicho  ilihali  Aruna Quadri  wa Naijeria akipambana na wachezaji wengine kumi na watano katika jitihada zake za kushiriki kwa mara nyingine katika mashindano ya dunia, yatakayoandaliwa nchini Ufaransa, mwaka huu. Aidha, wachezaji wengine wakiwamo; Olufunke Oshonaike na Segun Toriola wa Naijeria na Ahmed Saleh wa Misri pia watajitosa ukumbini kuwania kufuzu kwa mashindano ya dunia.