Maafisa wa upelelezi wa jinai wapanua uchunguzi wa mauaji ya Monica kimani, mshukiwa akifikishwa mahakamani

Maafisa wa upelelezi wa jinai wanaochunguza mauaji ya Monica Kimani ambaye mwili wake ulipatikana kwenye bafu la nyumba moja iliyoko mtaa wa kilimani jijini Nairobi wamepanua uchunguzi wao siku moja pekee baada ya mshukiwa mkuu wa mauaji hayo kufikishwa katika mahakama moja ya Kiambu.

Polisi walichukua alama za vidole na kulizuilia gari moja linaloaminika kutumiwa na mshukiwa mkuu Joseph Irungu, usiku ambapo Monica Kimani aliuawa. Gari hilo limesajiliwa katika jina la mwanahabari mmoja wa hapa nchini Jacque Maribe ambaye alijiwasilisha kwa maafisa wa upelelezi kwa mahojiano.

Haya yanajiri huku ibada ya wafu ya marehemu ikiandaliwa mjini Thika huku miito ikitolewa ya kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na mauaji hayo.Huzuni ulitanda katika uwanja wa Happy valley mjini  Thika, huku familia, jamaa na marafiki wakikusanyika kwa ibada hiyo ya wafu.Wabunge wanawake wameelezea wasi wao kutokana na ongezeko la visa vya mauaji vinavyowalenga wanawake.