Maafisa Wa Idara Ya Usajili Watishwa Kuondolewa Eastleigh

Tume ya utekelezaji haki sasa inahimiza kuondolewa kwa maafisa kadhaa wa idara ya usajili ardhi na serikali ya kaunti ya Nairobi kuhusiana na kuwahamisha kwa nguvu wafanyibiashara kutoka soko la wazi la Eastleigh. Mwenyekiti wa tume hiyo Otiende Amollo alifichua kwamba ardhi ambako soko hilo lilikuwa iliuziwa wastawishaji wawili kinyume cha sheria. Aidha alitoa wito kwa wizara ya ardhi kuharakisha mfumo wa kuhifadhi takwimu kwa njia ya kielektroniki ili kuepusha visa kama hivyo siku za usoni. Amollo alikosoa lililokuwa baraza la jiji la Nairobi kwa kukabidhi ardhi moja kwa watu kadhaa na kuwahamisha wafanyibiashara kwa nguvu kutoka kipande cha ardhi cha ekari 1.26. Ripoti kutoka kwa tume hiyo inaangazia jinsi maafisa kadhaa wa lililokuwa baraza la jijiji la Nairobi waliwasaidia wastawishaji wa kampuni ya kimataifa ya Alpha Traders and Gold Lime International kununua kipande hicho cha ardhi kinyume cha sheria. Kwenye mapendekezo yake tume hiyo ya utekelezaji haki ilihimiza kufidiwa kwa wafanyibiashara hao kwa hasara waliopata. Tume hiyo pia imehimiza kukomeshwa ustawishaji wa aina yoyote kwenye ardhi hiyo na kuhimiza kuwepo kwa makubaliano ya wadau wote kati ya sekta za kibinafsi na ile ya umma.