Maafisa Wa Chama Cha Madaktari Wakashifu Gavana Rutto Kwa Mashambulizi

Maafisa wa chama cha madaktari na wataalam wa meno KMPDU, wamemkashifu gavana wa Bomet Isaac Rutto kwa kumshambulia afisa mmoja wa chama hicho baada ya kuingia kwa nguvu kwenye mkutano wa faragha wa chama hicho uliokuwa ukiendelea katika hoteli ya Fair Hill mjini  Bomet. Yadaiwa gavana huyo alimshambulia mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho  Samuel Oroko. Maafisa wa chama hicho cha madaktari walikuwa mjini Bomet kujiondoa kwenye makubaliano yaliyokuwa yameafikiwa baina ya wahudumu wa afya na serikali ya kaunti ya Bomet siku ya jumamosi ambayo yalikuwa yamependekeza nyongeza ya mishahara ya asilimia 15 kwa wahudumu hao wa afya. Chama hicho kimedai kuwa Erick Kibet aliyetia saini makubaliano hayo, sio afisa wake na hivyo makubaliano hayo hayakuwa halali. Katibu mkuu wa chama cha KMPDU  Ouma Oluga alikariri kuwa hawatayumbishwa na vitisho dhidi ya maafisa wa chama hicho. Hata hivyo, gavana  Rutto amekanusha madai hayo akisema kuwa hamiliki bunduki yoyote.