Maafisa saba wapatikana na hatia katika kashfa ya ‘wheelbarrow’ Bungoma

Maafisa saba wa zamani wa serikali ya kaunti ya Bungoma jana waliagizwa kulipa faini au kuhudumu vifungo mbali mbali vya jela na mahakama moja ya Kakamega, baada ya kupatikana na hatia ya kuongeza gharama ya Rukwama yaani wheelbarrow. Mshtakiwa wa kwanza, John Juma Matsanza ambaye alikuwa afisa wa uhasibu katika kamati ya utoaji zabuni, alihukumiwa pia kutokana na mashtaka mawili ya kuacha makusudi kuzingatia sheria kuhusu usimamizi na kusababisha gharama kinyume cha sheria ya mwaka 2003 kuhusu vita dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi. Hivyo basi alitozwa faiuni ya shilingi elfu- 800 kutokana na makosa hayo mawili au kuhudumia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Wengine ni pamoja na Ayub Tuvuka China, Howard Lukadilu, Oscar Onyango Ojwang’, Arlington Shikuku Omusieni, Jacqueline Nanjala Namukati na Reuben Rutto ambao kila mmoja alihukumiwa kwa mashtaka mawili ya kuacha makusudi kuzingatia taratibu zilizowekwa na pia mwongozo kuhusiana na ununuzi na pia utoaji zabuni.  Waliagizwa kulipa shilingi elfu-600  kila mmoja  au kuhudumia kifungo cha miaka miwili gerezani. Mahakama ilipuuzilia mbali ombi la mawakili wao kutaka waachiliwe kwa dhamana hadi watakapowasilisha kesi za rufani.